Share news tips with us here at Hivisasa

Wakongwe kutoka eneo bunge la Kitutu Chache wameiomba serikali ya kitaifa kutafuta mbinu mwafaka ya kuwalipa pesa za msaada ambazo ni za uzeeni wanazozipokea kila baada ya miezi miwili.

Wakongwe hao wanataka kutumiwa fedha hizo kupitia kwa simu za mkononi, baada ya kubainika kuwa wanasumbuka kutembea hadi ofisi za chifu kila wakati.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika eneo la Sombogo walipokuwa wamekutana kupokea pesa hizo, wakongwe hao waliiomba serikali kuwatumia pesa hizo kupitia kwa simu zao ili kujali maslahi ya uzee wao.

Wakiongozwa na Shadrack Achachi, mwakilishi wao, walisikitikia jinsi wengi wao husumbuka wanapoziendea pesa hizo huku wakitembea safari ndefu.

"Baadhi yetu hatuna nguvu za kutembea, naona tuwe tunatumiwa pesa kupitia M-pesa kwa vile tuko na simu na tumejiandikisha kwa M-pesa,” alihoji Achachi.

"Naomba wanaosimamia pesa hizi kujali maslahi yetu,  hatuna nguvu ya kutembea safari ndefu na huenda nisije hapa tena kwani ni safari ndefu na ya kuchosha," alilalama Moraa Mose.