Wafugaji Kisii wametakiwa kukoma kuwaamini madaktari ambao hawajahitu kutoa matibabu kwenye mifugo wao.
Haya yanajiri baada ya visa vya wanyama kuendelea kufa kwa sababu ya ushauri mbaya kutoka kwa madaktari ambao hawajahitimu kuendelea kuripotiwa katika kaunti hiyo.
Wakulima wametakiwa kuwa makini wanaponunua dawa za mifugo na kukoma kuwatumia madaktari wa mifugo ambao hawajahitimu wala kuidhinishwa na kamati ya madaktari wa mifugo nchini (KVB).
Wenye mifugo wamekuwa na mtindo wa kununua dawa kutoka maduka ya kuuza dawa za wanayama ambazo wahudumu wao mara nyingi hawana hati za kuonyesha kuwa wamefuzu kuuza dawa za mifugo.
Akiongea katika ofisi yake siku ya Jumanne, mkurugenzi mkuu katika Idara ya huduma za matibabu ya wanyama, Dkt Benard Moenga alisema kuwa wafugaji wengi katika kaunti ya Kisii wamekuwa na mazoea ya kununua dawa kutoka katika Agrovet na kutafuta huduma za tiba ya mifugo kutoka kwa watu ambao hawajafuzu au madaktari wa kutumia matibabu ya kiasili.
“Wahudumu kwenye maduka hayo hawana ujuzi wa kitaalamu kuwashauri wafugaj jinsi ya kutibu wanyama na mara nyingi hutoa ushauri wa kubahatisha na huenda hukafanya wanyama kufa,” alisema Moenga.
Dkt Moenga aliwashauri, wenye mifugo kutafuta ushauri wa kitaalamu kutoka kwenye idara yake ili wawe na ufahamu wa kutosheleza mahitaji ya kimatibabu kuhusiana na mifugo wao na kuhakikisha kuwa mifugo wao wanapewa huduma ilio safi.
Aidha, alisema kuwa sio lazima wafugaji kuenda hadi ofisi za idara hiyo kwenye kaunti kwa masuala mepesi, na kuwataka kutumia vizuri maafisa wa mifugo walioko katika kila lokesheni ili kuwapa utatuzi wa masuala husika.
Moenga pia aliwataka walaji nyama kuwa makini na kuhakikisha kuwa nyama wanayonunua kwenye bucha imekaguliwa.