Mkurungenzi wa shirika la Feeding Future amesema kuwa mazao yanaweza kuwa bora na idadi yake kuongezeka iwapo wakulima watatumia mbinu za kisasa za kilimo.
Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, Vanessa Bennet alisema baada ya shirika lake kuanzisha mradi wa kuwapa wanafunzi chakula katika shule ya msingi ya St Brendans iliyo kwenye kaunti ya Nakuru, wameweza kuwahamasisha wazazi wao ambao ni wakulima kuhusiana na mbinu mpya za ukuzaji wa vyakula, hatua ambayo anasema tayari imezaa matunda kwani wameshuhudia ongezeko la mazao.
“Mwaka wa 2010 na 2011, tulianza kuwapa vyakula wanafunzi wa Shule ya St Brendans kwa kuwa wanafunzi walikuwa wanazimia kila mara kutokana na njaa walipokuwa shuleni. Baada ya hilo, tulianza kuwasaidia wazazi wao kwa kuwapa mafunzo kuhusiana na njia bora za kuendeleza kilimo,” alisema Bennet.
Aliongeza, “Tangu tulipoanzisha mradi huo, makundi matatu ambayo tumekuwa tukifanya kazi nayo yamebadili njia ambazo yamekuwa yakifanya kilimo na sasa yameweza kupata mazao zaidi,” alisema Bennet.
Kulingana naye, ingawa wakulima wa Kenya wanakabiliwa na matatizo kama vile mabadiliko ya hali ya anga, wanaweza kudumisha usalama wa chakula iwapo watajumuisha teknologia mpya pamoja na mradi wa unyunyizaji wa maji kwa mashamba.
Kwa upande wake, Peterson Githinji, mwalimu mkuu wa shule hiyo amesema utafiti wa kilimo unaofanyika katika shule hiyo ya msingi ya St Brendans umewapelekea wakulima kugundua mambo mengi muhimu baada ya kupata mafunzo ya jinsi ya kuimarisha kilimo chao.
“Tuliwapa wakulima hao mbegu bora ya mahindi na hapo wakaanza kuyapanda na kufikia sasa, wengi wameweza kupanda eka mzima. Hilo linamaanisha kwamba wanapata chakula cha kutosha nyumbani kwao. Kutokana na hilo, tunaona kuwa kuna usalama wa chakula nyumbani na shuleni,” alisema Githinji.
Aliongeza, “Tumeweza kujumuisha wataalamu wa kilimo na tunafanya kazi kwa pamoja na wizara ya kilimo. Kwa Pamoja, tumegundua kuwa mambo mengi yanaweza kufanyika katika eneo hili.”
Mwalimu huyo alisema uzalishaji wa vyakula nchini uliadhirika baada ya ghasia zilizojiri baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 na kutokana na hilo, baadhi ya familia zilikosa chakula na ndiposa iliafikiwa kwa mradi huo wa kuwapa wanafunzi chakula shuleni kuanzishwa.