Vikundi mbalimbali vya wakulima wa mboga katika kaunti ya Nyamira wako na kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali ya kitaifa kuwanunulia wakulima hao mashine ambazo zitatumika kukausha mboga zao ili kuzuia kuharibika kwa mboga hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika mji wa Nyamira, mwenyekiti wa mradi huo wa ununuzi wa mashine hizo katika kaunti ya Nyamira Kinari Orenge, alisema mashine hizo zilinunuliwa na serikali kuu ikishirikiana na nchi ya Sweden pamoja na chuo kikuu cha Kisii ili wakulima wasiwe wanapata hasara mboga zao zinapoharibika na kusema mashine hizo zitakausha mboga hizo ili ziweze kuuza wakati wowote bila kuharibika.
Mradi wa ununuzi wa mashine hizo ambao utakuwa wa kunufaisha wakulima wa kaunti ya Nyamira ili kukuza biashara zao uligharimu shillingi millioni 1.6.
Wakati huo uo, Naibu Gavana wa kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo aliyehudhuria hafla hiyo alisema serikali ya kaunti hiyo itaendelea kuwasaidia wakulima hao kwa kuwapa mbegu za mboga ili waweze kukuza biashara zao.
“Tutawapa mbegu za mboga mbalimbali ili mfanye kilimo hicho na kusaidika nyakati za usoni,” alisema Nyarobo.
Mwenyekiti wa wakulima wa mboga kaunti ya Nyamira Evans Obare, aliomba wakulima kushirikiana pamoja ili kuendeleza biashara zao za mboga na kujiimarisha kimaisha.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na mkuu wa chuo kikuu cha Kisii Profesa John Akama ambaye alisema juhudi za biashara zitasaidia kupunguza umaskini katika jamii ya mkisii.