Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakulima kutoka Kaunti ya Kisii wameombwa kuanza kufanya kilimo mseto cha mimea ili kuepusha jamii kutokana na baa la njaa.

Akiongea siku ya Jumatatu ofisini mwake, anyesimamia idara ya kilimo katika Kaunti ya Kisii Vincent Sawe, alisema kuwa wakazi wa Kisii wamekuwa wakishuhudia upungufu wa chakula cha kutosha, kwasababu ya kutegemea chakula kutoka kwenye aina moja ya mmea.

Sawe alisema kuwa ni vyema wakulima kutoka Kaunti hiyo ya Kisii, wajihusishe na upandaji wa mimea ya kustahimili hali ngumu ya kiangazi kama inayoendelea kwa sasa katika eneo ya Gusii.

"Ningependa kuwahimiza wakulima kupanda mimea kama vile miogo, mtama na viazi tamu. Nawaomba mukome kuwekeza asilia mia ya mashamba yenu katika kilimo cha mahindi kwani jambo hilo ndilo limechangia pakubwa kwa kuwa na chakula kisichotosheleza wakazi," alisema Sawe.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Gavana wa Kaunti ya Kisii Bwana James Ongwae kuwataka wakulima pamoja na wafugaji kutoka kaunti hiyo, kuzingatia kilimo mbadala, na kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo. 

Ongwae alikuwa akizungumza kwenye kongamano lililowakutanisha washika dau wa masuala ya kilimo katika taasisi ya mafunzo ya wakulima ya ATC mjini Kisii.

Kaunti ya Kisii imekuwa miongoni mwa kaunti ambazo zinaendelea kukuwa kwa kiwango cha haraka sana kulingana na ripoti ya shirika moja lisilo la kiserikali.

Hata hivyo, changamoto ambayo imekuwa mwiba kulingana na baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka sehemu hiyo ni kupungua kwa vipande vya ardhi ambavyo vinaendelea kufanyiwa ugavi.