Watu wanaoishi na ulemavu kutoka Kaunti ya Kisii wametakiwa kujiunga kwenye makundi ili kupata mkopo kutoka ili kujiendeleza katika maisha yao.
Wale walio na vipaji pia wametakiwa kutembelea ofisi ya Idara ya wanaoishi na ulemavu kuweka wazi uwezo wao uwe wa kiufundi au wa michezo kwa kuwa idara hiyo sasa ina nia na azimio la kuendeleza maisha yao.
Akiongea katika ofisi yake siku ya Jumatano wakati wa kupokea nguo za kuvaliwa na watu wenye ulemavu wa ngozi dhidi ya makali ya miale ya jua, mkurugenzi mkuu wa watu wanaoishi na ulemavu Isaac Rogito, alisema kuwa kuna hela ambazo zimetengwa mahususi kwa watu walio na ulemavu na sharti watu hao wajitokeze ili kupewa pesa hizo kwa kujiandikisha na idara hiyo.
“Watu wanaoishi na ulemavu wanapojiunga kwa makundi inakuwa raisi kwao kupokezwa pesa za mikopo ili kujiendeleza. Nitaendelea kutoa ujumbe huo kupitia kwenye mikutano ambayo huwa baina ya watu wanaoishi na ulemavu,” alisema Rogito.
Rogito aliktoa furaha yake kufuatia kupewa ripoti kuwa wengi wa watu wanaoishi na ulemavu sasa wanaendelea kufanya kazi yao bila kutegemea pesa za kuomba mitaani.
Alitoa mfano wa kijana ambaye amekuwa na talanta ya kutengeza na kukarabati vitimagurudumu na hata kujenga vidhibiti kama vile breki za mikono kuwafaa walemavu kinyume na vitimagurudumu nyingi ambazo zina breki zao upande wa chini na hudhibitiwa kwa miguu.