Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi ametishia kuwachukulia hatua walimu wakuu katika shule zote eneo la Changamwe ambao shule zao hazitafanya vyema katika mtihani wa kitaifa.
Akizungumza wakati wa mazungumzo ya maendeleo iliyofanyika katika shule ya msingi ya Kwa Hola, Changamwe, Omar alisema kuwa walimu wakuu wavivu ambao hawataweza kuongoza shule zao kufanya vyema hawatavumiliwa.
"Kwa kuwa jukumu letu ni kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapata elimu bora na wala siyo bora elimu. Walimu wakuu ambao shule zao zitaonekana kuzembea na kushindwa kufanya vyema katika mitihani ya kitaifa watahamishwa kwingineko au kuombwa kustaafu mapema," alisema Omar.
Kulingana na mbunge huyo, walimu wakuu kote nchini wametwikwa majukumu ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wao wanafanya vyema masomoni kwa minajili ya msingi imara.
Mwinyi aliwahakikishia wakazi wa Changamwe kwamba maendeleo kamili yatapatikana kabla ya kipindi chake kumalizika mwaka wa 2017 na kabla ya kuwaomba nafasi nyingine.
Aliwahakikishia wakazi hao kwamba mipango ya kujenga upya kumbi za kijamii za Bomu na Kaloleni zimekamilika na kuongeza kwamba visima na umeme zitasambazwa maeneo yote kabla ya 2017.
Aliongeza kwamba tayari kima cha Sh20 milioni zimetengwa kujenga shule ya upili ya Bomu huku Sh15 milioni kujenga shule ya upili ya Mwijabu huku akiwahimiza vijana kuanzisha miradi ya maendeleo badala ya kusubiri usaidizi kutoka kwa serikali.
Licha ya sekta ya elimu kukumbwa na mizozo ya mgomo wa walimu kwa muda wa wiki nne, Omar alisema kuwa ni sharti wanafunzi wa kidato cha na nne na darasa la nane wajitahidi kujiandaa kwa mitihani yao ya kitaifa na kusubiri serikali kupata suluhu ya mgomo wa walimu nchini.
Wakati huo huo, Omar alishutumu wakuu wa kampuni ya EPZ kwa kuendeleza kile alichokiita ukoloni mambo leo miongoni mwa wafanyikazi wake.
"Sitaweza kuvumilia wananchi wakiendelea kugandamizwa na waajiri wachache ambao lengo lao ni kupata faida kubwa bila kujali maslahi ya wafanyikazi,” alisema Omar.
Aliongeza kwamba atahakikisha wafanyikazi wa EPZ iliyoko Changamwe wanarudishwa kazini na pia maslahi yao ya kikazi kushughulikiwa ipasavyo.