Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amewaomba walimu wakuu wa shule za kaunti hiyo kujenga bweni za shule kwa kuzingatia sheria za ujenzi.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano afisini mwake mjini Kisii, Maang alisema ni muhimu bweni za shule kujengwa kwa kuzingatia sheria za ujenzi ili kupunguza mikasa ya moto na kujeruhiwa kwa wanafunzi wakati wa mikasa hiyo.

Maangi alisema kuwa kila bweni la shule linastahili kuwa na milango mingi na dirisha nyingi ili mkasa wa moto unapotokea, wanafunzi waweze kupata fursa ya kutoroka.

Hii ni baada ya bweni la shule ya upili ya wavulana ya Moi Gesusu kushika moto siku ya Jumanne na kusababisha hasara.

Alisema pia kila bweni la shule sharti liwe na bidhaa vya kuzima moto ili kupunguza hasara zinazotokana na mikasa ya moto.

Aidha, naibu gavana huyo aliahidi kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii itawasaidia wanafunzi waliopoteza bidhaa zao wakati wa mkasa huo wa shule ya Moi Gesusu.

“Serikali ya Kaunti ya Kisii imetoa pole kwa wanafunzi wale walifumaniwa na mkasa wa moto katika shule ya upili ya Moi Gesusu. Tutasaidia wanafunzi wale waliopoteza bidhaa zao. Nawaomba walimu wakuu wa shule wanapojenga bweni za shule wawe wanafuata sheria za ujenzi na kuzizingatia kikamilifu,” alisema Maangi.