Chama wa walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri nchini KUPPET katika Kaunti ya Mombasa kimekiri kuwa walimu hawatarudi shuleni hadi pale serikali itakapowalipa mishahara na marupurupu yao ya asilimia 50 na 60.
Kulingana na Katibu wa chama hicho katika kaunti hiyo ya Mombasa Bi Lynette Kamadi, hatua ya mahakama kuitaka Tume ya kuajiri walimu nchini TSC kuwalipa walimu mishahara yao inafaa kutekelezwa bila pingamizi.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu baada ya kufanya maandamano, Kamadi alisema kuwa mahakama ilitoa uamuzi halali kwa kuzingatia sheria na haki za walimu kutokana na dhulma walimu wamekuwa wakipitia tangu jadi, na akaitaka serikali kukoma kuwahadaa walimu kila mwaka.
“Sisi kama walimu wa nchi hiyo tumeamua hatutarudi shule kisa na maana tumenyimwa nyongeza ambayo tulipewa kihalali na sheria na uamuzi wa koti. Wale mahakimu hawakufanya makosa yoyote walipotupatia nyongeza kwa sababu tunastahili hiyo nyongeza,” alisema Kamandi.
Katibu huyo wa chama cha KUPPET katika Kaunti ya Mombasa alisema kuwa viongozi wa serikali na wale wa tume ya kuajiri walimu nchini lazima wazingatie maslahi ya walimu na kulitatua tatizo lao kwa wakati mwafaka la sivyo hawatarudi shuleni kabla ya kupewa nyongeza yao.
“Tume ya kuajiri walimu na viongozi wengine wa serikali wajue ya kwamba sisi kama walimu tutarudi shuleni haraka iwezekanavyo iwapo watatulipa,” alisema Kamadi.
Aidha, wamewashinikiza wazazi kutowaruhusu watoto wao kwenda shuleni hadi pale mgomo utakapositishwa baada ya serikali kuwapa walimu nyongeza yao ya misharahara na marupurupu ya asilimia 50 na 60.
Mgomo huo wa walimu umeingia juma la pili sasa huku serikali kupitia wizara ya elimu nchini na tume ya kuajiri walimu, ikitoa vitisho vya kuwafuta walimu kazi iwapo hawatarudi shuleni.