Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Walinzi katika maeneo mengi ya Kaunti ya Kisumu wameitaka serikali kuwapa silaha dhabiti ili kuimarisha ulinzi katika maeneo yao ya kazi.

Mmoja wa walinzi kutoka kikosi cha Macros Securicor kilicho na ngome yake mjini Kisumu, Robert Wanjala alisema pana haja ya serikali kuruhusu kampuni na makundi ya kiusalama nchini kumiliki silaha za kisasa kama vile bunduki ili kuwawezesha kudhibiti usalama vikamilfu.

Wanjala alisema kuwa baadhi ya walinzi kwenye maeneo mengi wangali wanatumia silaha hafifu zilizopitwa na wakati licha ya mambo ya usalama nchini kuchukua mfumo mpya.

''Tungelipenda serikali kuruhusu kampuni za ulinzi nchini kumiliki silaha ili kuwapa walinzi hao fursa ya kudhibiti ulinzi na kuimarisha usalama katika maeneo yao ya kazi,'' alisema Wanjala.

Akizungumza na Wandishi wa habari katika eneo analofanyia kazi la Nyalenda, mjini Kisumu Jumamosi asubuhi, Wanjala alisema kuwa wahalifu na magaidi wana silaha hatari ambazo hawawezi kukabiliana nao wakati wa uvamizi.

Aidha, mlinzi huyo alidokeza kuwa baadhi ya kampuni nyingi na makundi ya ulinzi katika maeneo mengi nchini zingali zinatumia vifaa hafifu kama vile; rungu, mishale na hata wengine mikono mitupu kwa maafisa wao katika kudumisha ulinzi katika maeneo yao ya kazi.