Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Ni furaha kwa watu zaidi ya milioni 2.5 nchini ambao walikuwa wameathirika kwa kubugia pombe kwani watapata matibabu ya bure.

Akiongea siku ya Jumatano katika mkutano wa machifu na manaibu wao katika eneo bunge la Nyaribari chache, mwenyekiti wa chama cha kupambana na dawa za kulevya nchini Nacada John Mututho alisema wale ambao wameathirika na pombe watapata matibabu ya bure katika hospitali za hapa nchini ili waweze kurejelea maisha yao ya kawaida.

“Serikali itawasaidia wale walioathirika kwa kubugia pombe kila siku kwa uzoefu. Watu hao watatibiwa bila malipo kwani tunahitaji eneo la Kisii na Kenya nzima iendee mbele,” alisema Mututho.

Aliongeza: "Tumetenga pesa ambazo zitawashughulikia wale watu ambao wameathirika na haturuhusu pombe haramu kuendelea kuuzwa hapa nchini.”

Wakati huo huo, Mututho aliomba machifu na manaibu wao wawasilishe majina ya watu walioathiriwa na pombe katika vijijini kwa serikali ya kitaifa ili washughulikiwe.

Mututho alishukuru kampeni ya kupambana na pombe haramu ambayo inaendelea nchini ili maisha ya watu kuwa katika hali nzuri.

“Utumizi wa dawa za kulevya na pombe haramu ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine mwilini. Mtu akizoea huwa vigumu kuacha kutumia dawa hizo lakini kwa sasa hatutaruhusu pombe haramu kamwe,” alisema Mututho.

Wakati huo huo, aliomba vyombo vya habari kuelimisha wakenya kuhusu hatari za kutumia dawa za kulevya kila siku kama njia mojawapo ya kupunguza utumizi wa dawa hizo katika jamii.

“Kampeni hii ambayo imefanyika hapa Kisii isiwe ya mwisho. Nawaomba muendelee kuelimisha jamii kuhusu hatari za utumizi wa pombe haramu,” alisisitiza Mututho.