Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kutokana na ongezeko la visa vya kudorora kwa usalama katika maeneo ya Uasin Gishu wadau, hasa wamiliki wa hoteli za kifahari mjini Eldoret, wanataka kupewa usalama na maafisa wa polisi waliojihami.

Ombi la wamiliki hao limewadia siku chache tu baada ya wabunge wa kaunti kuanza kujadili hoja ya usalama ambayo iliwasilishwa bungeni humo na kiongozi wa walio wachache Bw Ramadhan Ali.

Kulingana na wamiliki hao, kuna uwezekano wa wahalifu kuanza kuvamia hoteli hizo hivyo basi kuna haja ya ulinzi wa wateja wao kuimarishwa.

Wakizungumza siku ya Jumatano, Wafanyibiashara hao walidai kuwa iwapo usalama wa hoteli zao hautaimarishwa, sekta ya utalii na hoteli kwa jumla itaanza kuyumbayumba katika maeneo lengwa.

Wamiliki hao walisema idadi kubwa ya hoteli zao ziko katika maeneo ya viungani mwa mji wa Elodret na maeneo mengine ambayo yako nje ya miji.

Wadau hao walisema ikizingatiwa umbali wa mahoteli yao kutoka katikakati mwa mji wa Eldoret, kuna haja ya usalama kuimarishwa katika hoteli husika.

Wakiongozwa na Bw Joseph Wainana, ambaye ni mmiliki wa hoteli ya Queens Garden mjini Eldoret, walisema wako tayari kushirikiana na serikali katika maswala ya usalama wa hoteli zao.

Walisema kwamba iwapo usalama utaimarishwa, biashara yao itachangia pakubwa katika mapato ya kaunti zao na taifa kwa jumla.

“Kama vile tumekuwa tukishuhudia hali ya usalama katika eneo hili, kuna haja ya usalama wa wateja wetu ambao wengi wao ni watu mashahuri kuimarishwa,” alisema Wainaina.