Wanachama wa muungano wa Cord kutoka Kaunti ya Mombasa, wamewasuta baadhi ya viongozi kwa kuonekana kukosoa viongozi wa chama hicho hadharani katika hafla za kisiasa wakiwataka kujiuzulu kutoka kwenye uongozi wa mwungano huo.
Wanachama hao ambao waliongea katika ukumbi mmoja mjini Mombasa siku ya Jumatatu, walisema kuwa baadhi ya viongozi wa chama hicho cha upinzani wamekuwa na mtindo wa kutoa maneno ya kuukashifu muungano huo na kudai kuwa baadhi yao huenda wanatumiwa na mrengo wa serikali kuuvuruga muungano huo.
Akiongea kwa niaba ya wanachama hao, Mwenza Mwinyi, alisema kuwa hata kama kila kiongozi ana haki ya kutoa maoni yake, ni vyema zaidi viongozi ambao wanawajibikia chama kutafuta njia ya kuita wenzao na kuwaelezea kile ambacho wanahisi hakijawaridhisha, badala ya kuwakashifu baadhi ya vinara wa muungano huo.
Mwenza aliwataja baadhi ya wabunge pamoja na wawakilishi wadi fulani ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakimkosoa gavana wa kaunti ya Mombasa Bwana Hassan Joho hadharani.
“Ningependa kutoa wito kwa viongozi hao kuwa wazi na kukabili masuala vile yalivyo. Viongozi wanapaswa kumuendea kiongozi yeyote ambaye wanaona kuwa hajawaridhisha ili kutatua mambo kwa njia ya hekima,” alisema Mwinyi.
Shutuma hizo zinakuja siku chache tu baada ya baadhi ya viongozi wateule kutoka kaunti ya Mombasa kuonekana kumkosoa gavana Joho kwa utendakazi wake.