Mwaniaji wa uenyekiti wa muungano wa 'Jubilee Alliance Party' (JAP) katika jimbo la Nakuru, amewataka wafuasi wa vyama vya URP na TNA kujiunga pamoja na kudhihirisha umoja kwa lengo la kuupa nguvu muungano huo kama sehemu ya matayarisho ya uchaguzi mkuu wa 2017.
Akizungumza mjini Nakuru katika kikao na wanahabari siku ya Jumamosi, James Karemi, alitoa wito kwa viongozi wa TNA katika kaunti nzima ya Nakuru kuzika tofauti zao, kama wanataka ufanisi wa chama hicho siku zijazo.
“Sisi tumeitika wito wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, na kwa hivyo, kama Kaunti ya Nakuru tuko nyuma yao, na wasiogope chochote kwani tuko ndani ya JAP,” alisema Karemi.
Alisema kuwepo kwa umoja kati ya viongozi na wafuasi wa vyama hivyo viwili, ndiko kutawafanya rais na naibu wake kusalia katika ikulu kwa vipindi vingine vitatu, na kugonga miaka 20 ya utawala.
Aidha, alitoa changamoto kwa waliohusika katika kupeana taarifa za uongo kwenye mahakama ya ICC huko Hague kujitokeza hadharani na kueleza ukweli ili kuiwezesha mahakama hiyo ya kimataifa kutenda haki kwa Naibu Rais William Ruto na mtangazaji Joshua arap Sang.
Nelson Omondi kiongozi wa JAP kutoka Homabay, alisema Jubilee haingejipata katika ikulu pasi na uwepo wa Ruto.
“Watu wa Nyanza tunaombea Ruto ushindi katika Hague, manake bila Ruto hatungepata waziri mkuu kutoka eneo la Victoria. Ruto pia amesaidia pakubwa katika Jubilee kuingia Ikulu. Kwa hivyo, wacha tumpe nafasi, na Uhuru akiondoka tunampatia kura kama rais wa Kenya,” alisema Omondi.