Mkewe gavana wa kaunti ya Kisii Elizabeth Ongwae akishirikiana na shirika la msalaba mwekundu amewapa viatu wanafunzi 280 wa shule za msingi kutoka familia zisizojiweza kifedha.
Waliofaidika ni wanafunzi kutoka wadi ya Monyerero eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini kaunti ya Kisii.
Akiongea katika wadi hiyo siku ya Jumanne Bi Ongwae alisema ataendelea kufadhili wanafunzi katika wadi zote 45 za kaunti ya Kisii. Aliongeza kwamba atasaidia haswa wale ambao familia zao hazijiwezi ili ili kuwapunguzia changamoto ambazo huwakumba wakiwa shuleni.
“Nimeanzisha mradi huu wa kuwapa viatu wanafunzi wa shule za msingi ili kuwasaidia wale wanaotoka familia ambazo hazijiwezi kifedha. Tunataka wao pia waweze kuendelea na masomo yao bila tashwishi kama wenzao darasani," alisema.
Wakazi ambao pia ni wazazi katika shule za wadi ya Monyerero walimpongeza Bi Ongwae huku wengi wakimwomba kuendelea na ufadhili huo.
“Watoto wanakwenda shule bila viatu hasa msimu huu wa mvua huenda wakapata magonjwa haswa huko vyooni na pia ugonjwa unaoletwa na baridi,” Evans Ongori, mkazi mmoja alisema.