Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosomea taaluma ya ualimu katika Kaunti ya Kisii wametishia kuandamana ikiwa serikali haitawaongeza walimu mishahara yao kwa juma moja lijalo.

Tishio hilo limetolewa baada ya serikali na tume ya kuajiri walimu nchini TSC kususia kuwalipa walimu jambo ambalo limepelekea maandamano kuenda kushuhudiwa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili mjini Kisii, mwenyekiti wa chama cha Kenya Association of Education Students katika kaunti ya Kisii, John Otao, na katibu wa chama hicho Kevin Mamboleo, waliomba serikali kuheshimu uamuzi wa mahakama na kuwalipa walimu nyongeza yao ya mishahara kwa juma moja lijalo la sivyo waungane na walimu kuandamana.

“Sisi ndio walimu wa siku zijazo. Tunaomba serikali ya Kenya iwalipe walimu nyongeza yao,” alisema Otao.

“Hatumbelezi serikali na tume ya TSC kuwalipa walimu ila ni haki ya walimu kulipwa mishahara jinsi mahakama ilivyoagiza. Ni aibu sana wakati serikali inaonekana kutoheshimu mahakama kumanisha serikali imekiuka agizo la mahakama,” alisema Mamboleo.

Mwenyekiti huyo aliomba serikali kuheshimu katiba na kutekeleza yale inahitajika kuyafanya.

Matamshi hayo yaliungwa mkono na mwenyekiti wa chama cha Uraia Trust katika kaunti ya Kisii, Hamisi Oyunge, ambaye alisema serikali ya Jubilee iko katika uongozi kufuatia uamuzi wa mahakama uliotolewa na kuomba serikali kuheshimu uamuzi wa mahakama dhidi ya walimu.