Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi wanne wa shule za upili tofauti wametiwa mbaroni katika eneo la Lari wakiwa na dawa za kulevya.

Akidhibitisha kisa hicho siku ya Jumanne, afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Lari, Inspekta Peter Ouko alisema wanne hao walitiwa mbaroni mnamo saa nne asubuhi pale walipokuwa wakielekea shuleni.

Alieleza kuwa wanne hao walimiliki misokoto minne ya bangi na pombe kali iliyokuwa imewekwa kwa chupa na kuchanganywa na soda.

Ouko alieleza kwamba wanafunzi hao walishukiwa na polisi waliokuwa wakishika doria katika eneo hilo na walijaribu kuhepa lakini polisi waliwashika na baada ya kuwafanyia msako wa haraka, waliweza kuwapata na dawa hizo za kulevya.

Afisa huyo alisema wanne hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Lari wakisubiri kupelekwa mahakamani.

Hata hivyo, Ouko alisema kwamba wanne hao watasaidia uchunguzi dhidi ya kuwakamata wale wanaowauzia dawa hizo.

Alisema kwamba polisi wamepata habari ambazo zitawasaidia kuwatia mbaroni wale wanaoendeleza uovu miongoni mwa watoto wa shule.

"Uchunguzi wetu unaendelea kubaini wale wanaohusika katika kuwauzia wanafunzi dawa za kulevya. Hata hivyo, ningewaomba wazazi wachukuwe jukumu wakati huu shule zinapofunguliwa kwa kuwapeleka watoto wao mpaka shuleni kuzuia utovu wa nidhamu unaoshuhudiwa wakiwa peke yao,” alisema Ouko.