Wanafunzi wametakiwa kuwa waadilifu kwenye likizo yao ili kuepuka anasa na maovu katika jamii shule zinapofungwa.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Lwala iliyoko katika Tarafa ya Chemelil kwenye Kaunti Ndogo ya Muhoroni, Edison Mwaro aliwataka wanafunzi kuacha matembezi ya kiholela na badala yake kurejelea masomo.
''Shule zikifungwa tunawashauri wanafunzi kusalia manyumbani wakiwasaidia wazazi kazi za nyumbani na kusoma ili wasije kusahau kwa haraka silabasi,'' alisema mwalimu huyo mkuu akiwahutubia wazazi na wanafunzi kabla ya shule hiyo kufungwa mnamo siku ya Jumatano.
Pia mwalimu huyo aliwaonya wazazi dhidi ya kuwahusisha wanafunzi kwa kazi zinazoweza kuwaathiri kiakili.
Mwaro alidokeza kuwa nyakati za likizo wanafunzi katika maeneo mengi hupatikana wakirandaranda sokoni wakiwa wametumwa na wazazi kununua na kuuza bidhaa.
''Ni vizuri kama wazazi kufuatilia kila hatua ya mtoto maishani. Matembezi ya watoto kwenye soko bila sababu muhimu huchangia sana utovu wa nidhamu miongoni mwao,'' aliongeza kusema mwalimu Mwaro.
Aidha, alisema kuwa hali ya wazazi kushindwa kuwazuia wanao kurandaranda nyakati za likizo hufanya wengi kukosa kurudi shuleni wakati shule zinapofunguliwa baada ya wanafunzi wa kike kupachikwa mimba za mapema.