Share news tips with us here at Hivisasa

Mkewe gavana wa Kaunti ya Kisii Elizabeth Ongwae amewaomba wanawake wanaougua ugonjwa wa fistula kujitokeza kutibiwa bila malipo kwanzia tarehe 12 mwezi huu hadi tarehe 26 katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya wanawake wanaougua ugonjwa huo katika Kaunti ya Kisii.

Matibabu hayo yatatolewa kupitia shirika la Freedom From Fistula Foundation Flying Doctors Society wakishirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kisii.

Akizungumza siku ya Jumatano katika zahanati ya Tongeri iliyoko katika wadi ya Bokimonge, Kaunti ya Kisii, Elizabeth Ongwae aliwaomba watu kujitokeza ili kutibiwa ugonjwa huo ambao umeonekana kuwasumbua watu wengi ulimwenguni.

Alisema hapo awali walipoandaa kambi ya kuwatibu watu katika hospitali ya Kisii, wanawake 83 waliweza kutibiwa huku wakitarajia kuwatibu watu wengi zaidi wakati huu.

“Tunaomba wanawake wengi waweze kujitokeza ili watibiwe ugonjwa huu wa fistula maana watapata tiba bila malipo. Ugonjwa huu umekuwa ukisumbua watu wengi katika sehemu mbalimbali za nchi ndio maana tumeandaa kambi ambayo itakuwa katika Hospitali ya rufaa ya Kisii ili kuwasaidia walioathirika,” alisema Bi Ongwae.