Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idadi kubwa ya wanaume imekuwa ikijitokeza mjini Eldoret kunufaika na huduma ya VCT ya usiku ili kujua hali yao ya HIV.

Huduma hiyo ambayo inaendelezwa na shirika la Hope Worldwide Kenya hulenga maeneo ambako kuna kumbi nyingi za starehe pamoja na maeneo ambako kuna madanguro.

Akizungumza siku ya Ijumaa, afisa wa maswala ya nyanjani wa shirika hilo Bw Pascal Mabele alisema kwamba lengo la huduma hiyo ni kufikia watu ambao hawana nafasi ya kutembelea vituo vya VCT mchana.

“Tuligundua kuwa watu wengi haswa wanaume hawana nafasi ya kutembelea vituo vya VCT mchana. Hii ndio sababu tulianzisha huduma hii. Tangu tuanze huduma hii, watu wengi wamenufaika,” alisema Mabele.

Bw Mabele alifichua kuwa mbali na kuhudumia walengwa, huduma hii imewafanya wanaume wengi kujua umuhimu wa kutumia mipira ya kondomu.

“Kupitia kwa shirika hili tumekuwa tukitoa ushauri kwa watu kuhusu mbinu za kujikinga na ugonjwa wa ukimwi, ambapo tunatoa uhamasisho kuhusu mbinu za kujikinga. Kwa sasa matumizi ya kondomu yameongezeka miongoni mwa wanaume,” alisema Mabele.

Mabele alisema huduma hiyo pia imekumbatiwa na makahaba katika maeneo tofauti haswa katika barabara ya Oginga Odinga ambayo ni maarufu kwa biashara hiyo.

“Moonlight VCT imesaidia watu wengi sana, hasa wale ambao huogopa kutembelea VCT mchana. Mimi pia nimenufaika kwa sababu imenisadia kujua hali yangu ya HIV,” alisema Kahaba mmoja mjini humo.