Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kundi la wanawake katika eneo la kabete wametangaza kuanza kampeni dhidi ya ukahaba.

Wanawake hao walilalamika kuwa waume wao wamekuwa waathiriwa na pia mwenendo huo unawapotosha wanao.

Akihutubia kundi la akina mama la 'Kabete Women Movement' siku ya Ijumaa, mwenyekiti wa kundi hilo Bi Faith Kiharo, alisema kuwa ukahaba ulikuwa umekita mizizi katika eneo hilo kwa muda wa miezi miwili.

Alisema kwamba pindi tu vita dhidi ya pombe haramu vilipoanza, biashara hiyo haramu ilikuwa inatekelezwa usiku na mchana.

Kiharo alisema kwamba ukahaba ulikuwa unawavutia waume wao ambao hutumia pesa zote wanapotoka kazini katika danguro hizo.

Alisema kuwa tabia hii ilikuwa inatekelezwa na wanawake wa umri mkubwa na pia wasichana wadogo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa watoto wa eneo hilo pia walikuwa wanaathirika kwa kupotoshwa kwa kuwa ukahaba ulikuwa umeanza kuwa jambo la kawaida, linaloendelezwa mchana.

Alikashifu wanaowakodishia makahaba hao nyumba na kuruhusu watekeleze tendo hilo.

Alisema kwamba akina mama walikuwa wamechoka na pia kugadhabika na tabia hii ambayo ilikuwa imeshaanza kuwafanya wazee kutowajibika nyumbani.

Kiharo alisema ukahaba huo umevunja ndoa nyingi, akitoa mfano wa wanawake 12 walio katika kundi lao.

Kiharo alisema wanawake wa kundi hilo walikuwa tayari kuanza vita vikali dhidi ya uhalifu wa aina hiyo kwa kuwa juhudi zao kurepoti kwa chifu wa eneo hilo hazija badilisha lolote.

"Tumeanza kampeni na tumewaita akina mama wote na pia wanadada katika eneo hili ili tuweze kukomesha ukahaba katika eneo hili. Ni dhambi na pia ni hatia kisheria na hatutaruhusu tabia hii," alisema Kiharo.

Kiharo alisema wataungana na maafisa wa usalama kuwashika makahaba na kuwapeleka kwa polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Aliwaomba wenye nyumba za kukodisha wawafurushe kutoka nyumba hizo la sivyo watazivunja ili kuwatoa makahaba hao.

“Kampeni hii itaanza usiku wa leo na tutahakikisha tunalinda waume wetu dhidi ya ukahaba. Wanaotekeleza uovu huu si wakazi wa eneo hili bali wamekodisha nyumba katika eneo kadhaa wanapoendeleza tabia hiyo,” alisema Kiharo.