Share news tips with us here at Hivisasa

Wanawake kutoka Kisii wametakiwa kujiandikisha ili kupata vitambulisho kama njia mojawapo ya kupata nafasi za kazi kwa urahisi.

Akizungumza siku ya Alhamisi, mkurugenzi mkuu wa idara ya usajili katika Kaunti ya Kisii Thomas Rosana, alisikitia idadi kubwa ya jinsia ya kike hasa wale ambao wameolewa ambao hawana hati hizo muhimu.

Aliwaomba wanaume kuhakikisha kuwa wanawahimiza wake wao kupata vitambulisho hivyo ili kuonyesha uhalisia wao na kujiepusha kutokana na kushukiwa kuwa wageni kutoka nchi nyingine.

Rosana alisema kuwa jinsia ya kike imejitenga kwa muda mrefu huku akisema ni sharti wanawake waache kubaki nyuma na kujiepusha kuishi nyakati za zamani na kuishi kisasa.

Aliwapa changamoto kuanza kujisajili kwani ni haki yao kupata hati hizo ikizingatiwa kuwa siku hizi kila mtu lazima awe na kitambulisho ndio apewe kazi.

Aidha alisema kuwa kina mama huwa na wakati mgumu wanapopoteza waume wao kwani wao husumbuka kutafuta hati za kuzaliwa kwa vile wengi hawana vitambulisho hali ambayo huwachelewesha watoto wao kupiga hatua maishani.

"Nawaomba wanawake waanze kuchukua vitambulisho ili waweze kupata ajira na vile vile kujiepusha kusumbuana na maafisa wa polisi kwa kukosa hati hiyo," alisema Rosana.

Alisema kuwa ana matumaini kuwa ujumbe huo utaendelea kutiliwa maanani kupitia vikao na mikutano ya machifu na ile inayoandaliwa na ofisi hiyo ya kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuwa na hati hizo.

Alisema kuwa wanawake wameanza kuchukua hatua ya kujisajili japokuwa kwa mwendo wa kinyonga.