Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa Kaunti ya Kisii wenye umri wa miaka zaidi ya 16 na hawakuwahi kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya shule za msingi wametakiwa kujiandikisha na idara ya kushughulikia elimu ya watu wazima kutimiza ndoto zao.

Haya ni kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa elimu ya watu wazima katika Wilaya ya Kisii ya Kati Bi Olpha Nyakundi.

Mkurugenzi Nyakundi alisema kuna umuhimu wa watu wazima pamoja na wale vijana ambao hawakufanikiwa kumaliza shule kwa sababu mbali mbali wa kujisajili ili kupata ujuzi na utaalam kupitia idara hiyo maarufu kama Ngumbaru.

Akiongea siku ya Jumatano katika ofisi zao mpya ambazo zimekamilishwa kujengwa hivi majuzi, Bi Nyakundi aliwapongeza wengi wa watu wazima ambao wamekuwa wakijiandikisha katika mpango huo wa kupata elimu na kuwataka kuendelea kuonyesha moyo huo na pia kuwafahamisha wenzao ambao bado hawajajiunga nao kufanya hivyo.

Alitaja ukosefu wa walimu, madarasa, vyombo vya kufundishia miongoni mwa vingine kama baadhi ya changamoto kuu wanayopitia na kuiomba serikali kuu kuyashughulikia masuala hayo ambayo aliyataja ni yenye umuhimu mkubwa mno kwao.

Kwa sasa mpango huo wa masomo wa watu wazima pamoja na vijana unafanyiwa katika baadhi ya madarasa yaliyomo Shule ya Msingi ya Kisii ambapo wana zaidi ya wanafunzi 90 ambao wamejiandikisha kufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane na inatarajia kuwa idadi hiyo itaendelea kuongezeka.