Wawakilishi wa wadi katika kaunti ya Nyamira wamelahumiwa vikali na wananchi kwa kutumia pesa nyingi kujifurahisha kimaisha na mambo ya kibinafsi.
Hii ni baada ya kubainika kuwa wawakilishi hao walitumia shilingi millioni 18 kusafiri hadi nchi za ng’ambo, million tano kwa safari za kuenda mji wa Mombasa, na kukabidhiwa shillingi alfu 10 kama marupurupu kwa kila kikao katika bunge.
Haya ni kwa mjibu wa ripoti ambayo ilitolewa na ambayo iliangazia utimizi wa fedha katika kila kaunti.
Wakizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, wananchi hao, wakiongonzwa na aliyekuwa mwenyekiti wa baraza za awali wilayani Nyamira David Makori na afisa Paul Kengere walisema pesa za kaunti hiyo zinaenda kwa mifuko ya watu binafsi badala ya kufanya maendeleo.
“Hizi pesa wanazozitumia ni za maendeleo sasa hivi katika kaunti ya Nyamira hakuna maendeleo yamefanywa twende wapi, tusimamiwe na serikali gani ambayo itajali maslahi yetu?” aliuliza Makori.
“Badala ya kutengeneza Nyamira nayo iweze kuinuka zaidi kimaendeleo na kibiashara, wanaenda na kuinua miji mingine haswa mikahawa kwani tuliwachagua kwa kujifurahisha maisha yao pekeee badala ya kutufanyia maendeleo sisi twahitaji maendeleo,” alidokeza Kengere.
Wakati huo huo, wananchi hao waliomba gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kukaa na wawakilishi ili kupanga jinsi watawafanyia maendeleo wananchi wa kaunti hiyo kwani wamesumbuka pakubwa.
“Tunaomba sisi tufanyiwe maendeleo, hayo mambo mengine ya kujifurahisha na maisha sisi hatutaki kamwe na tumekataa,” alisema Mary Omweri, mkaazi.