Wafanyibiashara wawili katika mji wa Kisii walitiwa mbaroni na Askari wa Kaunti ya Kisii siku ya Jumatano baada ya kupatikana wakitupa taka katika mji huo kinyume na sheria za mazingira.
Akiongea wakati wa kuwatia mbaroni wawili hao, mwenyekiti wa kikundi cha Minto Youth Group ambacho kinashughulikia usafi katika mji wa Kisii ambaye aliambatana na Askari hao Kepha King’oina alisema kuwa waliwatia mbaroni wawili hao ili wawe funzo kwa walio na tabia hizo za kutupa taka katika mji wa Kisii na viunga vyake kiholela.
Aidha, King’oina aliwaonya walio na tabia kama hizo za kutupa taka mahali popote huku kukiwa na pipa za kutupa taka hizo akisema kuwa hawatalegeza kamba kwa yeyote atakaye patikana pahala hapastahili kwani ni kuvunja sheria.
“Wawili hao watakuwa funzo kwa wengine walio na tabia kama hii kwa kuwa kuna mazoea ya watu kutupa taka mahali kiholela kwa kizingizio kuwa kuna wale wakufanya kazi ya kufagia mji huu,” alihoji King’oina.
Kwa mujibu wa King’oina, kikundi cha Minto kinafanya kazi kila siku ya kusafisha mji wa Kisii na ni wajibu wa kila mkazi kuhakikisha mji huo ni safi kila wakati.
Kwa sasa amewaomba walio na tabia hiyo kukoma akioneza kuwa sheria imeanza kuchukua mkondo wake kwani wasipokoma wengi watajipata mashakani.
Wawili hao walifikishwa katika mahakama ya Kisii huku wakitarajiwa kusomewa mashtaka ya kutotunza mazingira.