Share news tips with us here at Hivisasa

Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya kimatifa ya mtoto wa kike duniani, wazazi wameshinikizwa kuwalinda watoto wao ili kuona kwamba hawakumbwi na changamoto za hedhi.

Akiongea mjini Mombasa baada ya kuwakabidhi sodo wasichana wa shule mbalimbali za msingi katika eneo la Likoni, Mwakilishi wa Kike katika kaunti ya Mombasa Mishi Mboko alisema kwamba kuna haja ya mtoto wa kike kuangaziwa vyema ili kumkinga na changamoto za hedhi.

Kulingana na Mboko wanafunzi wengi wa kike katika kaunti hiyo hukwepa masomo yao shuleni wanapopitia hali hiyo huku wengine wakilazimika kutumia pamba ama vitambaa vya nguo kama sodo ili kuwawezesha kujikimu na hali hiyo.

Mboko ameyashinikiza mashirika ya kijamii kujitokeza na kushirikiana na viongozi mbalimbali wa kike katika kumsaidia mtoto wa kike ili kuafikia malengo yake ya masomo na kuzisaidia jamii zao katika siku za usoni.

"Wasichana wetu wanapitia changamoto nyingi sana wakati wakipitia kipindi cha hedhi kwa sababu wengi wao hawana uwezo wa kunua sodo na hata wazazi wao pia hupitia changamoto. Tumeamua kama wanawake kuungana na kuwasaidia watoto wetu wa kike katika siku kama hiyo ya kuadhimisha siku ya msichana dunia ili wao pia waweze kusaidiaka," alisema Mboko.

Kiongozi huyo ameahidi kuzuru shule mbalimbali katika kaunti hiyo ili kuwaelimisha walimu na wazazi jinsi ya kuwasaidia wanafunzi wa kike kujitokeza na kuanza kutumia sodo wakati wa hedhi na kuepukana na changamoto.