Wazee kutoka katika kijiji cha Riat, Kaunti ya Kisumu wamewaonya vijana dhidi ya kuuza mashamba ambayo ni uridhi wa jamii.
Inasemekana kwamba vijana wanaomiliki mashamba huuza mashamba hayo kiholela baada ya kukabidhiwa stakabadhi za kumiliki mashamba kutoka kwa wazazi.
Wazee hao walikuja pamoja siku ya Jumanne wakikashifu tabia hiyo wakisema kwamba vijana wanao tekeleza biashara hiyo wananuia kuleta mizozo ya mashamba katika jamii huku wakipoteza uridhi wao.
''Ardhi ndio uridhi wa kipekee kwa jamii zetu na ukoo nyingi zingali zinaenzi utunzi wa ardhi ya ukoo kama mojawapo ya maadili ya kudumisha utamaduni. Hivyo basi, ni sharti tabia ya uuzaji mashamba kiholela katika jamii ikomeshwe,'' alisema Dalmas Mbidha wakati wa kikao.
Aidha, wazee hao walidai kuwa vijana hao hutumia pesa wanazopata baada ya kuuza mashamba hayo kwa kujihusisha na raha na ulevi, bila kuzingatia tahadhari za matokeo.
Walisema kuwa wanashirikiana na serikali ya Kaunti ya Kisumu kuwashauri vijana kushiriki katika miradi ya kimaendeleo ili kupata riziki na wala siyo kutegemea kuuza ardhi.
Aidha, wazee hao waliwataka vijana hao kuyatumia mashamba yao kwenye kilimo ili kuzalisha mapato.