Mmawamme mmoja alisababisha kicheko mahakamani baada ya kudai kwamba uvutaji wa bangi humwezesha kula.
Mtuhumiwa huyo kwa jina la Samuel Njoroge alikuwa amepatikana na gramu tisa za bangi katika eneo la bahati usiku wa Julai 10 katika eneo la Bahati katika Jimbo la Nakuru jambo ambalo lilimsababisha kukamatwa na maafisa wa polisi kabla ya kupelekwa katika kituo cha polisi cha Bahati.
Akijitetea katika mahakama moja ya Nakuru mbele ya hakimu mkuu Doreen Mulekyo siku ya Alhamisi, mshukiwa huyo mwenye umri wa makamo aliambia mahakama kwamba inambidi yeye kuvuta bangi ili kupata hamu ya kula chakula, jambo ambalo lilimfanya hakimu huyo kuangua kicheko.
“Inanibidi kuvuta bangi ili nipate hamu ya kula chakula kwani nisipovuta huwa siwezi kula zaidi ya vijiko vitatu,” alisema Njoroge.
Njoroge aliomba mahakama hiyo kumsamehe huku akisema kwamba atatatufa njia mbadala ya kujipatia hamu ya kula.
“Naomba mahakama hii inisamehe kwani ata bangi niliyopatikana nayo ilikuwa ni kiasi kidogo mno. Naahidi kutafuta njia nyingine ya kuniwezesha kula chakula,” alisema Njoroge.
Aliongeza kwamba asingalikuwa akivuta bangi afya yake ingekuwa imedhoofika mno.
Mshukiwa huyo atabaki kizuizini na atajua hatima yake mnamo tarehe Juni 26, 2015.