Mwakilishi wa wadi ya Gesima, Ken Atuti, amemuomba mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire na mwenzake wa eneo bunge la Borabu Ben Momanyi, kutoa pesa za kukarabati Shule ya msingi ya Nyansimwamu, iliyoko kwenye mpaka wa maeneo hayo.
Akiongea siku ya Alhamisi alipoitembelea shule hiyo, Atuti alidai kuwa wabunge hao wawili wamekataa kuitikia wito wa kukarabati shule hiyo.
Kulingana na Atuti, juhudi zake na za mwakilishi mwenzake wa wadi ya Nyansiongo, Jackson Mogusu, za kutaka usaidizi kutoka kwa hazina ya ustawi wa maeneo bunge CDF, kutoka kwa maeneo bunge hayo, hazijafaulu kwa sababu ya swala la mpaka.
“Nawaomba wabunge wetu Bosire na Momanyi kuingilia kati na kuisaidia shule hiyo kwa kukarabati paa na kuta za madarasa. Kamati za hazina ya CDF kwenye maeneo bunge hayo zimekuwa zikidanganya tunapofuatilia swala hilo,” alisema Atuti.
Wakati uo huo, Nyameino alifungua rasmi madarasa mawili yaliyokuwa yamejengwa na serikali ya kaunti ya Nyamira.