Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mmoja wa Polisi katika kitengo cha trafiki amezua kioja leo (Jumatano) asubuhi alipotaka kuingi kwa lazima katika gari moja ya taksi mjini Kisii.

Kisa hicho kiliwasababisha madereva wa kituo hicho kilichoko karibu na Supamaketi ya Shivling mkabala na mkahawa wa kifahari wa New Zonic kutaka kuchukua hatua ya kumchapa Polisi huyo kwa kudai kuwa kitendo chake ni kinyume na sheria.

Kwa mujibu wa mmoja wa madereva hao Charles Mokaya, alidai kuwa Polisi huyo wa trafiki alianza kuingia katika mojawapo ya magari yao huku akitaka kumtoa dereva aliyekuwa ndani kwa fujo, hali ambayo iliwakera baadhi yao na kutaka kumchapa.

“Nilimwona afisaa aking’ang’ana kufungua moja ya magari yetu ambako madereva wengine hawakufurahishwa maanake gari hilo lilikuwa limeegezwa. Sio vizuri hata kidogo ikiwa afisaa wa trafiki kuvunja sheria,” alihoji dereva Mokaya.

Madereva hao ambao walikuwa wameanza kujikusanya pamoja na watazamaji wengine waliokuwa wakipita walighadhabishwa na kitendo hicho huku wakiwaomba Maafisa kuwa na utaratibu wa kusuluhisha jambo linapozuka miongoni mwa madereva na wahudumu wengine wa barabara.

Kisa hicho kiliacha wengi na masuali ikizingatiwa kuwa ni majuzi tu afisa mmoja wa trafiki alidaiwa kumpokonya dereva funguo za gari na baadaye kusababisha ajali kwa kuwaua wanafunzi na mfanyakazi wa taasisi ya Sayansi ya Teknolojia ya Gusii (GIT) ambapo ilizua ghasia zilizodumu kwa siku nne.