Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Uchukuzi katika barabara ya kutoka eneo la Keroka kuelekea mjini Kisii ulisimamishwa kwa muda baada ya mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya upili ya Kegati kugongwa na gari siku ya Jumatano.

Wanafunzi wa shule hiyo walizuia magari kupita barabarani humo wakilalamikia kugongwa kwa mmoja wao ambaye alikuwa anavuka barabara ya kuingia kwa lango la shule hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo kutendekeka, mwalimu mkuu wa shule hiyo Innocent Siro alisema mwanafunzi huyo alinusurika kifo kwa kugongwa na gari na anaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii.

Wakati huo huo, mwalimu huyo mkuu alikosoa serikali na sekta ya uchukuzi kwa kutoweka matuta katika barabara hiyo, ili kuzuia magari kuendeshwa kwa kasi.

Kufikia sasa utulivu umerudi katika barabara hiyo huku wanafunzi wa kidato cha nne wakiendelea na mtihani wao wa kitaifa.

“Mmoja wa wanafunzi wangu aligongwa na gari aina ya probox wakati alikuwa anavuka barabara kuja shuleni, lakini Mungu alimsaidia na akanusurika kifo. Nimetoka hospitalini sasa hivi na mwanafunzi huyo anaendelea kushughulikiwa kimatibabu,” alisema Siro.

Aliongeza “Tumekuwa tukiihitaji matuta lakini hakuna lolote limefanyika na naomba sekta husika kujali maslahi ya wanafunzi na kutuwekea matuta katika barabara hii.”