Akina mama wanaougua ugonjwa wa fistula wamehimizwa kujitokeza na kupata matitabu maalum ya ugonjwa huo katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani mjini Mombasa.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, baada ya kuzinduliwa kwa kituo cha matibabu cha ugonjwa wa fistula mjini Mombasa, mkuu wa Idara ya Afya katika kaunti ya Mombasa Binti Omar, aliwaomba wanawake wajitokeze wapate matibabu.
Omar alisema kwamba kuzinduliwa kwa kituo hicho kutasaidia pakubwa kutibu ugonjwa huo unao wasumbua akina mama wengi na kuongezea kuwa serikali ya kaunti hiyo itafanya kila juhudi kuimarisha kituo hicho.
“Serikali ya kaunti iko tayari kuimarisha kituo hiki ili kuona kwamba akina mama wanaougua ugonjwa wa fistula wanapata matibabu maalum. Tunafahamu kuwa wengi wa akina mama hususan wale wa mashinani wanapitia changamoto nyingi kutokana na ugonjwa huu lakini sasa tiba imepatikana,” alisema Omar.
Aidha, alisema kwamba wizara yake itahakikisha kuwa akina mama wajawazito wanashughulikiwa kwa ungalifu wakati wa kujifungua ili kukinga uwezekano wa akina mama kukumbwa na maradhi ya fistula.
Omar amewataka wazazi na akina mama kujitokeza kwa wingi na kutembelea kituo hicho ili kupata ushauri nasaha pamoja na matibabu maalum ili kuona kwamba hali zao za kifya hazikumbwi na changamoto.
Omar aliwaonya akina mama wajawazito dhidi ya kujifungua nyumbani na kuwashauri kuvitembelea vituo vya afya ili kuepuka kukumbwa na maradhi ya fistula.
“Tafadhilini akina mama ukiwa wakati umefika wakujifungua tafadhali tembelea vituo vya afya upate usaidizi zaidi kutoka kwa wahudumu wa afya ili ujifungue vizuri,” alisema Binti.