Baadhi ya akina mama waliokuwa wagema na wanywaji wa pombe katika Wadi ya Bahati, eneo bunge la Bahati wameamua kuacha biashara hiyo na kuhakikisha wanaanza maisha yao upya.
Akina mama hao zaidi ya 50 walikutana katika ukumbi wa kanisa la PCEA Ngwataniro Bahati siku ya Alhamisi, ambapo walikuwa wameita Mwakilishi wa Wadi ya Bahati Bw Peter Nderitu Mwangi maarufu kama Birishiba, pamoja na wahubiri wawili ili kuwapa mwongozo wa jinsi wanavyoweza kuanza maisha yao upya baada ya kuacha kuuza au kunywa pombe.
Pia akina mama hao walielezea kufurahishwa na hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza pombe haramu iangamizwe, wakikariri jinsi pombe haramu imekuwa mnyororo ambao umesakama sio maisha yao tu, bali pia watoto, waume wao, na vile vile majirani yao.
Mmoja wao kwa jina Esther Wanjiru alisema: “Nilikuwa nakunywa pombe sana na kurudi nyumbani saa tano za usiku karibu kila siku. Nikifika nyumbani naanza kuchapa watoto ambao mara nyingi walikuwa wanalala njaa sababu hakukuwa na mtu wa kuwapikia.”
Naye Ruth Nyambura alieezea kwa masikitiko jinsi mumewe alivyokuwa amegeuka na kuwa zuzu, kwani alikuwa hata akienda haja kitandani na mara nyingi hakuwa anarudi nyumbani.
“Sasa najua nitafufua talanta yangu ya kuimba kama ataacha pombe tusaidiane maanake nitapata nafasi wa mazoezi” alisema Nyambura.
Mwakilishi Nderitu aliwataka kuunda kikundi walichoita Bahabiri Women Group, ambacho kitawasaidia kujikuza kimaendeleo na watakuwa wakikutana siku moja kwa mwezi.
“Tukiunda kikundi, mtaweza kupata cheti na kila mkikutana mnatoa pesa alafu tusaidiane kuwekeza katika ukulima wa green house kama kikundi kisha kila mmoja wenu akishapata ujuzi huo, mtasaidiana kuhakikisha nyinyi nyote mna vyumba hivyo nyumbani mwenu,” alisema Nderitu.
Pombe haswa aina ya chang’aa imekuwa ikipakiwa katika makaratasi yanayotumiwa kuuza sukari na kisha kusambazwa kwa wanunuzi na kwa mujibu wa polisi mmoja wa AP aliyeomba kutotajwa jina, kabla ya Rais Kenyatta kutoa agizo la pombe haramu kuangamizwa, Wilaya ya Nakuru Kaskazini ilikuwa na zaidi ya madanguro 300 ya kuuzia pombe hiyo haramu.