Kiongozi wa wachache katika bunge la Kaunti ya Nakuru Daniel Ambale amekanusha madai kuwa wawakilishi wadi wa Nakuru wamezembea katika kutekeleza jukumu lao la kuipiga msasa serikali ya kaunti.
Ambale amesema kuwa wawakilishi wadi wametekeleza kila jukumu la kikatiba wanalopaswa kutekeleza, na kuwa hawafai kulaumiwa kutokana na matumizi mabaya ya pesa na maafisa wa serikali ya kaunti.
Akiongea siku ya Jumatano afisini mwake, Ambale alisema kuwa ni makosa kwa viongozi na wananchi wa Nakuru kuwalaumu wawakilishi wadi kwa makosa yaliyotekelezwa na serikali ya kaunti.
“Kuna ngazi mbili za uongozi katika kaunti na inafaa watu wafahamu kuwa bunge la kaunti ni tofauti na seriklai ya kaunti. Kwa hivyo, kama serikali imetumia pesa ilizotengewa vibaya, sisi kama bunge la kaunti hatupaswi kulaumia,” alisema Ambale.
Aliongeza kuwa serikali ya kaunti chini ya Gavana Kinuthia Mbugua inajukumu la kuelezea ni kwa nini ilitumia pesa bila kupata idhini ya bunge la kaunti, na ni kwa nini kiasi kikubwa cha fedha kinatumiwa kulipa mishahara ya wafanyikazi kuliko kutumika katika kufadhili maendeleo.
“Kamati ya seneti imemuita gavana kuelezea hayo yote na sisi kama bunge la kaunti pia tutamuita gavana aje atuelezee kuhusu shtuma hizo kabla ya kutoa ripoti kamili ya kile kitakachofuatia,” alisema Ambale.
Ambale aidha aliwataka wananchi na mashirika ya kijamii kutekeleza jukumu lao la kuipiga msasa serikali kuliko kile alichokitaja kama kuwalaumu wabunge kila wakati.