Baadhi ya wakazi wa mji wa Kisii na viunga vyake wamewaomba Askari wa kaunti ya Kisii kuwajibikia kazi yao bila kupendelea mtu yoyote ambaye amepatikana kuvunja sheria za Kaunti ya Kisii.
Haya ni baada ya kijana mmoja ambye ni mhudumu wa bodaboda kushikwa na Askari hao siku ya Jumapili alipokuwa akipita katika barabara ya Mashauri-Kobil ambapo waendeshaji bodaboda hawastahili kupitia kufuatia sheria za kaunti hiyo.
Kwa mujibu wa wakazi walioshuhudia kisa hicho, Askari hao waliwachilia wengine kupita na kushika kijana huyo kwa madai ya kuwa hawamjui.
Kwa sasa wamewaomba Askari hao kuamua kama ni marufuku kutotumia barabara hiyo basi waendeshaji bodaboda wote wasiwe wanaruhusiwa, wala sio baadhi yao tu.
Momanyi Mokaya ni mmoja wa wakazi hao ambaye alisema amekuwa akishuhudia vijana wa kuendesha bodoboda wakihangaishwa na Askari hao wanapopita katika barabara hilo, jambo ambalo alisema huenda likasababisha ajali kwani waendeshaji hao huenda mwendo wa kasi wanapowaona Askari hao ili kuwakwepa.
“Vijana hawa wa kuendesha bodaboda wanafanya makosa kupitia hapa lakini kuna njia ya kisheria inayostahili kutumika kukabiliana nao badala ya kuharakishwa au kukimbizana, hali amabyo itaweza kusababisha ajali," alihoji Momanyi.
Kwa upande wa Askari hao, wamewaomba vijana hao kuheshimu sheria za barabara katika Kaunti ya Kisii ili kujiepusha na mambo kama hayo.