Huku biashara za kuanzisha vituo vya kuuza mafuta ya petroli, diseli na yale ya taa ikiendelea kushika kasi katika mji wa Kisii, kina pwagu na pwaguzi hawajaachwa nyuma.
Kumezuka madai kutoka kwa wahumu wa bodaboda kuwa baadhi ya vituo vimekuwa vikichanganya mafuta aina ya diseli na mafuta taa na kuwauzia baadhi ya wateja wao ambao hawana habari na kudhania kuwa mafuta ambayo wamewekewa ni ya aina ya petroli.
Kiongozi wa waendeshaji bodaboda kwenye steji ya Kisii Central SDA ya bodaboda za kuenda Nyatieko, Peter Mose, alisema kuwa wamekumbana na zaidi ya visa kumi vya wenye pikipiki kulalamikia aina ya mafuta wameuziwa katika kituo kimoja cha mafuta kilichoko viungani mwa mji wa Kisii.
Bwana Mose alisema kuwa yeye ni miongoni mwa wahasiriwa ambapo kwa wakati mmoja, aliweza kuwekewa mafuta hayo yaliyofanyiwa mchanganyiko maalumu, na baadaye kurudi kituoni na kutoa ripoti kwa wahudumu lakini walipuuza madai hayo.
“Nilijipata wakati mmoja naendesha pikipiki yangu nikaona haiendi kama ilivyo kawaida nikaashindwa ni mafuta yalikuwa yameisha au ni nini? Kuangalia kwenye tanki la mafuta, nikaona mafuta yamejaa, ikabidi nirudi kwenye kituo hicho nikawaelezea lakini wakakataa. Tusubiri mkuu wa kituo husika tumpe malalamishi yetu,” alisema Mose.
Juhudi za kutaka kumwona mmoja wa wasimamizi wa kituo hicho hazikuzaa matunda, kwani wahudmu wa kituo hicho walisema kuwa hakuwa karibu na alikuwa amesafiri.