Baraza la wazee wa jamii ya Agikuyu limekashifu mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kutokana na madai yake kuwa mashahidi katika kesi dhidi ya Naib wa Rais William Ruto walipokea mafunzo.
Baraza hilo lilisema matamshi hayo iwapo hayatadhibitiwa, yataadhiri hali ya amani inayoshuhudiwa kwa sasa katika eneo la bonde la ufa.
Kupitia kwa taarifa iliyotolewa na msemaji wa baraza hilo Gilbert Kabage siku ya Alhamisi, wazee hao walisema jamii ambazo zilihusika katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 zimezika tofauti zao katika kaburi la sahau na matamshi yasiyo na msingi hayafai kukubaliwa.
Alisema kuwa imechukua rasilmali nyingi kutoka kwa serikali, mataifa mbalimbali, viongozi wa kidini na mabaraza ya wazee kuleta umoja na kuhakikisha kuna hali ya amani.
Aliongeza kuwa kama wazee, hawataketi chini na kushuhudia Kuria akitoa matamshi kama hayo kupitia kwa vyombo vya habari.
Kabage pia ametaja hatua ya Kuria ya kusalia kimya na kisha kuzungumza baada ya kuona kwamba mahakama ya kimataifa ya jinai ICC imekubali kutumia ushahidi wa baadhi ya watu waliokuwa wameondoa ushahidi wao dhidi ya Naibu wa Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Arap Sang mbele ya mahakama hiyo kama ya unafiki.
“Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ambaye ameungama kuwa alikuwa kati ya waliotafuta mashahidi na kuwapa pesa ili watoe ushahidi wa uongo dhidi ya Ruto kule Hague ni mnafiki wa hali ya juu. Anajitafutia umaarufu wa kisiasa. Itakuwaje baada ya miaka minane atatjitokeza na kusema kuwa alitafuta mashahidi wa uongo?” alisema Kabage.
Msemaji huyo pia amepongeza wabunge ambao wamekuwa wakikashifu usemi wa Kuria hadharani na hata bungeni huku akisema kuwa kama wazee, wataendelea kuhubiri amani kote nchini .
“Tungetaka Kuria na wenye nia kama hiyo kutoka mkoa wa kati kufahamu kwamba amani na umoja tulio nao sasa hatutaki utatizwe na mtu ama kundi la wanasiasa wanaojitafutia umaarufu,” alisema Kabage.
Kwa upande mwingine, Kabage ametaka Wakenya kuendelea kuwaombea Naibu wa Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Arap Sang na pia kuuungana Pamoja bila ya kuzingatia makabila yao.