Mke wa Gavana wa Nyamira Bi Naomi Nyagarama ameanzisha mradi wa kuwafadhili wakazi wa kaunti hiyo mbegu aina mbali mbali za mimea kuwawezesha kuboresha maisha yao kiuchumi.
Mojawapo ni aina ya ndizi ya 'tissue culture' pamoja na mbegu mpya za viazi vitamu ambazo hukomaa kwa haraka huku Bi Nyagarama akisema mbegu hizo hazivamiwi kwa urahisi na wadudu wanaosababisha maradhi.
Hafla hiyo ambayo ilifanyika siku ya Jumanne, ilianzia katika eneo la Miruka, viungani mwa Nyamira ikiongozwa na Bi Nyagarama ambapo alisema kuwa atahakikisha mradi huo unasambaa kila sehemu ya kaunti hiyo.
Aliongeza kwamba mradi huo unadhamiria kuwapa nguvu kiuchumi kina mama pamoja na vijana hasa wale hawana kazi ili kuwaweka katika hali ya kujijali na kujitegemea maishani.
Aidha Bi Nyagarama aliwataka wakazi wote kutoka kaunti hiyo kujikusanya kwa makundi ili iwe rahisi kwa mradi huo kuwafikia kwa urahisi na aliwaomva wawe wakitumia miradi hiyo kujiendeleza.
Baadhi ya wakazi waliofaidika kutokana na mradi huo walimpongeza Bi Nyagarama kwa kuwafaa katika mradi huo ambapo walimtaka aendelee kuwafaa kwa miradi kama hizo katika siku zijazo.
Pia walitoa wito kwa viongozi wengine kutoka kaunti hiyo kufuata mfanao wa Bi Nyagarama kwa kuanzisha miradi zaidi ili kupunguza ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana.