Share news tips with us here at Hivisasa

Bunge la Kaunti ya Nyamira limepitisha mswada wa kuitaka serikali ya kaunti hiyo kuweka sheria ambazo zitatumika kusimamia madarasa ya chekechea katika shule za msingi hasa kwa walimu wanaofundisha madarasa hayo.

Hii ni baada ya kubainika kuwa wengi wa walimu ambao hufundisha madarasa hayo hulipwa mshahara mdogo wa Sh10,000 pesa ambazo hawawezi kuweka ili kuwasaidia katika siku za usoni.

Mswada huo uliofikishwa katika bunge la kaunti hiyo na naibu spika ambaye pia ni mwakilishi wa wadi ya Gachuba, Andrew Magangi, unahitaji serikali ya kaunti hiyo kuwa na sheria za kusimamia walimu wa chekeckea na kuhakikisha wanalipwa mshahara mzuri.

Mswada huo utahakikisha walimu wa chekechea wanalipwa mshahara mzuri ikilinganishwa na mshahara wa sasa na kuajiriwa na serikali ya kaunti ya Nyamira kikamilifu.

Mswada huo ulipitishwa siku ya Jumatano na idadi kubwa ya wawakilishi wa bunge la Kaunti hiyo huku wengi wakimtaka gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kuutia sahihi ili kuwa sheria.

“Niliona wengi wa walimu ambao wanatufundishia watoto katika darasa la chekechea hulipwa pesa kidogo ndio nikaleta mswada huu bungeni ili nao waweze kusimamiwa na serikali ya kaunti na kulipwa vizuri,” alisema Magangi.