Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu Daniel Chemno amewapa changamoto wakazi wa Eldoret kuhakikisha kuwa watoto wao wamepata chanjo ya polio.
Akizungumza siku ya Jumamosi mjini Eldoret wakati wa kuadimisha siku ya polio ulimwenguni, Chemno aliwahimiza wazazi kupata huduma za hosiptalini wakati wanapojifungua ili waweze kuelimishwa zaidi kuhusu ugonjwa huo.
Naibu gavana huyo alihimiza wale wanaoishi na walioadhirika na ugonjwa huo kuwapa ushauri na usaidizi unaostahili kama vile malazi bora, na kuwapa nasaha kuhusu hali yao.
"Wanaoishi na walioadhirika na ugonjwa huu wawape usaidizi na wasiwaache wateseke kwani wanahitaji kuishi kama wanadamu wengine,” alisema Chemno.
Aliongeza, "Mbali na chanjo ya polio, wazazi wanatakiwa kuhakikisha wanao wanapata chanjo zingine zote zinazopeanwa na idara ya afya."
Aidha, alisema kuwa wazazi ambao hukataa wanao wapewe chanjo na maafisa wa afya watachukuliwa hatua za kisheria.