Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kiwanda cha Sukari cha Muhoroni kimewaonya wanaoendesha biashara ya kupiga sukari nguru na kutaka wakulima kushirikiana na kampuni kudhibiti hali hiyo.

Kwenye ujumbe uliotumwa kwa wakulima kutoka kwa mkurugenzi wa bodi ya washikadau katika kampuni hiyo, Bw Lazarus Okumu wakulima katika eneo hilo walitakiwa kuisaidia kampuni hiyo kukomesha biashara hiyo haramu kwa kukoma kuuzia wafanyibiashara hao miwa ya kampuni.

Okumu alisema kwenye barua hiyo ambayo ilisomwa katika mkutano wa wakulima wa nnje maarufu kama Out Growers mnamo siku ya Jumamosi kwamba, wafanyibiashara hao wanalenga kutatiza uzalishaji wa kiwango cha sukari kwenye kampuni hiyo.

''Wakati kiwango kikubwa cha miwa kinatumiwa kutengeza sukari nguru, inaonyesha kwamba kuna hatari za kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa sukari kwenye kampuni hii ambayo inategemewa pakubwa kwenye uchumi wa kanda hii na taifa zima,'' alisema Okumu kwenye barua hiyo.

Peter Mataso ambaye ni mwanahisa kwenye kampuni hiyo alitaka kuwekwa mikakati maalumu ya kupambana na wafanyibiashara hao aliowataja kuwa maadui wakubwa wa viwanda vya sukari katika eneo la Nyanza.

''Kupambana na hawa watu ni lazima kampuni ishirikiane na wakulima ili kuimarisha vita hivyo dhidi ya watu hao ambao wengi wao sio wakulima, lakini wanataka kujinufaisha na bidhaa hiyo,'' alihoji Mataso wakati wa kikao hicho kilichoandaliwa katika uwanja wa soko la Songhor, Kaunti ya Kisumu.

Biashara hiyo imeenea sana miongoni mwa jamii za maeneo yanayokuza miwa Nyanza, huku ikiwa na soko sana ikizingatiwa kuwa wagema nao wanaitegemea pakubwa kutengeneza mvinyo.