Mwenyekiti wa bodi ya vyuo vinavyotoa mafunzo ya udaktari hapa nchini Prof Phillip Kariuki amesema chuo cha udaktari tawi la Kisii kitapanuliwa zaidi ili wanafunzi 2,000 kupata fursa ya kusomea katika chuo hicho ikilinganishwa na wanafunzi 800 ambao wanasoma katika chuo hicho kwa sasa.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika chuo hicho kilichoko katika mji wa Kisii, alipotembelea chuo hicho huku akiwa na afisa mwingine wa bodi hiyo Daniel Mwangi, Kariuki alisema taaluma zingine za masomo ya udaktari zitaongezwa katika chuo hicho ili wanafunzi wawe wanasomeshwa taaluma nyingi ikilinganishwa na zile zinasomeshwa katika chuo hicho.
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo alisema watafungua vyuo vingine vya kutoa mafunzo ya udaktari kwa kila kaunti hapa nchini ili wanafunzi wengi wapate fursa ya kusomea udaktari.
“Chuo hiki cha Kisii huwa kinafanya vizuri katika mitihani na tumeamua kukipanua zaidi ili tuhakikishe kuwa wanafunzi wamepata elimu ya kutosha ili viwango vya elimu kuinuka zaidi katika sekta ya udaktari,” alisema Kariuki.
Mwaklimu mkuu wa chuo hicho cha Kisii Getruth Apiyo alisema tayari mikakati imeimarishwa kikamilifu na kuafikiwa katika chuo hicho ili kuinua viwango vya elimu na kuanzisha kutoa mafunzo ya taaluma zingine ambazo zimeongezwa kutolewa katika chuo hicho.
“Tunawakaribisha wafanyibiashara walio na uwezo wa kujenga vyumba vya kulala vya wanafunzi kushirikiana nasi ili wanafunzi wa chuo hiki waweke makao yao katika nyumba hizo," alisema Apiyo.