Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mahakama kuu ya Mombasa imesimamisha kwa muda dhamana iliyopewa wasichana wanne wanaodaiwa kuwa na uhusiano na kundi la al-Shabaab hadi pale kesi hiyo itakapo sikilizwa.

Hii ni baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa kuwasilisha ombi la kufutiliwa mbali dhamana hiyo iliyopewa wasichana hao siku ya Jumatatu, wiki iliyopita.

Hakimu Richard Odenyo aliwatoza dhamana ya Sh500,000 kila mmoja, jambo lililopingwa na mwendesha mashtaka Daniel Wamotsa kutoka afisi ya mkurugenzi wa mashataka ya umma.

Akizungumza siku ya Jumatano Wamotsa alisema kuwa wasichana hao wanahusishwa na mashtaka mazito ya ugaidi hivyo basi hawapaswi kupewa dhamana.

Wasichana hao walikamatwa katika eneo la Elwak lililoko karibu na mpaka wa Kenya na Somalia Kaunti ya Garissa, wakidaiwa kuwa safarini wakielekea nchini Somalia kujiunga na kundi la al-Shabaab.

Watatu hao Ummulkheir Abdullah kutoka Zanzibar mwenye umri wa miaka 21, Mariam Said Aboud pamoja na Khadija Abubakar wenye umri wa miaka 19 wote kutoka Malindi wanadaiwa kuwa wanafunzi walioahidiwa ufadhili wa kimasomo, huku Halima Aden akikamatwa katika Kaunti ya Machakos kwa tuhuma za ugaidi.