Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameahidi kuzisaidia familia za watu watatu walipoigwa na radi katika Kijiji cha Mochorwa, wilayani Kenyenya.
Watatu hao walipigwa na radi siku ya Jumatatu wakati walikuwa wakijiandaa kwa sherehe ya mazishi ya mpendwa wao, huku mmoja akijeruhiwa na kunusurika kifo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne afisini mwake mjini Kisii, Gavana Ongwae alisema serikali yake itasaidia familia zilizoathirika pamoja na kugharamia mazishi ya walioaga dunia.
“Serikali yangu itahakikisha familia ambazo ziliwapoteza wapendwa wao zimesaidiwa kikamilifu maana kifo hiki hakikutarajiwa na ninawapa pole,” alisema Gavana ongwae
Ongwae pia aliahidi kugharamia gharama zote za hospitali za aliyenusurika kifo na kupelekwa katika Hospitali ya Kenyenya kwa matibu.
Aidha, Ongwae alisema serikali yake imejitayarisha vilivyo kupambana na mvua ya El Nino ambayo imeonyesha dalili ya kunyesha katika sehemu za Kisii.
“Serikali yangu pia itahakikisha hakuna watu wanajeruhiwa wakati wa mvua hii ya El Nino maana tumejitayarisha kupambana na visa vyovyote vinavyoweza sababishwa na mvua hiyo,” aliongeza ongwae.