Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema serikali yake imeimarisha mikakati kabambe ya kuhakikisha hakuna mkazi wa kaunti yake anaathiriwa na mvua nzito inayotarajiwa kunyesha ya El Nino.
Kulingana naye, serikali ya kaunti ya Nyamira imejitayarisha kupambana na changamoto zote zitakazosababishwa na mvua hiyo nzito huku akisema kila kitu kiko shwali na kuwahakikishia wananchi wa kaunti ya Nyamira kutokuwa na wasiwasi wowote kuwa wataathiriwa na mvua hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Nyamira, gavana Nyagarama alisema kuwa watashirikiana na sekta ya uokoaji pamoja na ile ya usalama kuhakikisha wananchi hawataathiriwa.
“Serikali yangu imejitayarisha kupambana na changamoto zitakazoletwa na mvua ya El Nino ili mtu yeyote asiaathiriwe vyovyote,” alisema Gavana Nyagarama
Aliongeza gavana: “Naomba kila mtu awe macho na mtu asifanye msaha kuwa hakuna mvua ya El Nino kilichotabiliwa kiko.”
Kamishena wa kaunti ya Nyamira Joshine Onunga alisema katika sekta yake ya usalama itashirikiana na serikali ya kaunti ya Nyamira kuhakikisha hakuna mtu anajeruhiwa na mvua hiyo.
Pia kamishena huyo aliomba wakazi weanaoishi katika sehemu zilizo za chini na kwenye mabwaga kuhama mara moja ili wasiathiriwe na mvua hiyo.
“Wakati huu tutawapa namba ya simu ambayo ni ya sekta ya usalama ili mkiona chochote kitokeacho dhidi yenu mnapiga ili kupata usaidizi,” alisema kamishena Onunga.