Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amekanusha madai ya baadhi ya wakulima kuwa shahawa aliyeyatoa kwa wafugaji wa ng'ombe katika kaunti hiyo yalikuwa mbaya.

Akiongea siku ya Alhamisi katika uwanja wa Gusii wakati wa kufungua maonyesho ya kilimo katika Kaunti ya Kisii, Gavana Nyagarama alikanusha madai hayo na kusema shahawa hayo yalikuwa ya gredi bora.

Alisema kuwa yeye ni mmoja wa wale walioyapata shahawa hayo na kuongeza kuwa ng’ombe wake alizaa ndama mwenye afya, kinyume na madai ya baadhi ya wakulima wanaosema kuwa  shahawa hayo sio bora.

“Mimi mwenyewe niliyapata na ng’ombe wangu alizaa ndama aliye na afya nzuri na nikamwita gavana kwa hiyo hayo ni madai tu ya watu fulani ambao hawataki maendeleo katika kaunti yetu,” alihoji Gavana Nyagarama.

Kwa upande mwingine Gavana Nyagarama aliwaomba wakulima kutoka kaunti  yake kuhudhuria maonyesho ya kilimo ya Kisii ili kupata mbinu mpya za kisasa za ukulima.

"Nawaomba wakulima wote kutoka Kaunti ya Nyamira kufika hapa kupata mafunzo ya ukulima bora ili waweze kujiendeleza," aliongezea Nyagarama.

Aidha, gavana huyo alisema kuwa serikali yake itaendelea kuhakikisha kuwa wakulima kutoka Kaunti ya Nyamira wataendelea kunufaika na miradi ya kuinua uchumi wa kaunti hiyo haswa katika sekta ya ukulima.