Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amemtaka Gavana wa kaunti hiyo Hassan Joho kujenga sehemu ya upasuaji katika zahanati zote za kaunti ili kuboresha huduma za afya kwa akina mama.

Akiongea katika mkutano wa wanawake wa hamasa mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mboko alisema kwamba wanawake wengi hususan wale wajawazito hupitia changamoto nyingi wakati wa kujifungua, na mara nyingi hao hutumwa katika Hospitali ya Rufaa ya Ukanda wa Pwani kwa upasuaji hali inayopelekea kuwa ngumu kwao.

Mboko alisema kwamba endapo zahanati za kaunti hiyo zitatengewa sehemu maalum za upasuaji, ili kuwasaidia wanawake wajawazito wakati kunapatokea jambo la dharura, basi hatua hiyo itasaidia pakubwa kuokoa watoto wachanga kwani huduma za afya katika kaunti hiyo zitaimarika mara dufu.

“Tunamuomba gavana wetu wa Kaunti ya Mombasa achukue hatua mwafaka ya kujenga sehemu maalum ya upasuaji katika zahanati zote za kaunti ili kuona kwamba wagongwa wa kufanyiwa upasuaji wanasaidika badala ya kupelekwa katika hospitali ya rufaa, na mgonjwa kucheleshwa kupata hudumu hiyo,” alisema Mboko.

Aliongeza kwamba ni sharti Gavana Joho aendeleze juhudi za kuboresha sekta ya afya hadi mashinani ili kuhakikisha kwamba sekta hiyo iliyogatuliwa inamfaidi wakazi mashinani.