Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amekashifu uharibifu unaoshuhudiwa na wanaokabiliana na tatizo la pombe haramu nchini katika operesheni iliyoanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta.
Akiongea katika Kanisa la SDA la Kaptembwo katika hafla ya kuufunga mkutano wa kanisa hilo uliodumu kwa muda wa wiki mbili, Gavana Mbugua alilalamikia mbinu ya baadhi ya viongozi wanaopambana na pombe haramu akidai wanakivunja sheria na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyibiashara.
Alisema kuwa licha ya tatizo la pombe haramu kuwa donda sugu nchini, ni vyema kutekeleza amri ya rais kwa kufuata sheria bila kudhuru au kuharibu mali ya yeyote huku akisisitiza kuwa sheria sharti ifuatwe na yeyote anayetekeleza shughuli hiyo.
Mbugua aliongeza kuwa Serikali ya Kaunti ya Nakuru inaunga operesheni hiyo kikamilifu na akaliomba kanisa kujiunga nao katika juhudi za kukabiliana na tatizo la pombe haramu ambalo limeathiri watu wengi na kuongeza uozo katika jamii.
"Rais wetu ametuonyesha mfano mwema katika kukabiliana na janga hili na ni jukumu letu kutafuta suluhisho la kudumu na hivyo tunaomba kanisa kutoa mchango wao kwa swala hili ili tuwe na jamii tunayojivunia," alisema Gavana Mbugua.
Mbugua pia alihimiza viongozi wote nchini kuendelea na juhudi za kupiga vita ugaidi ambao umelemaza sekta nyingi za uchumi kama utalii. Gavana Mbugua alikuwa ameandamana na Mbunge wa Nakuru Magharibi Samuel Arama katika hafla hiyo.
Shughuli ya kupambana na pombe haramu ilianza wiki iliyopita baada ya Rais Kenyatta kuamuru ianze rasmi na mara kwa mara imetekelezwa kwa uharibifu wa mali na wananchi ambao wamejawa na ghadhabu kubwa kuhusu madhara yanayoletwa na pombe hiyo.