Wazazi kutoka Kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Gavana James Ongwae kuahidi kuongeza pesa za kusaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kulipa karo.
Akizungumza mnamo siku ya Ijumaa katika uwanja wa michezo wa Gusii alipohudhuria maonyesho ya kilimo yanayoendelea katika uwanja huo ulioko mjini Kisii,Gavana Ongwae alikiri kuwa pesa za ufadhili katika bajeti ya 2015 na 2016 zilikuwa Sh5 milion kwa kila wadi na kusema bajeti ya mwaka ujao 2016 na 2017 zitaongezwa hadi Sh7.5 milioni kwa kila wadi.
“Tunahitaji kuhakikisha kila mwanafunzi amepata nafasi ya kuendelea na masomo yake ili tuinue viwango vya elimu katika eneo la Kisii na kila mwanafunzi asome,” alidokeza Gavana Ongwae.
“Mwaka uliopita kila wadi ilipokezwa milioni 3 mwaka huu tukaelewana na Wawakilishi wa wadi katika Kaunti yetu ambazo ni 45 kuongeza pesa za ufadhili hadi Sh 5 milion mwaka ujao pesa hizo zitakuwa Sh7.5 milioni kwa kila wadi,” alisema Gavana Ongwae.
Gavana Ongwae alisema kiini cha kuongeza pesa hizo kila wakati ni kufuatia changamoto za familia masikini hupitia na ongezeko la wanafunzi mayatima katika Kaunti ya Kisii.