Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria amemshtumu mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kwa kutoa matamshi ambayo huenda yakazua chuki miongoni mwa Jamii mbalimbali hapa nchini.

Hii ni baada ya Kuria kudai kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua aliwafunza na kuwalipa mashahidi wa uongo katika kesi dhidi ya Naibu wa Rais William Ruto.

Akizungumza kwenye makao makuu ya Kaunti ya Nakuru siku ya Jumatatu wakati wa shughuli ya kuanzisha rasmi safari ya kupeleka dawa kwenye vituo vya kimatibabu vinavyopatikana kwenye kaunti hiyo, Gikaria amemtaka Kuria kuelekea katika mahakama ya kimataifa ya jinai ICC endapo yeye ni shahidi.

“Matamshi ya Kuria yawezafanya watu kufikiria mambo ya kuvurugana na ni Jambo la kusikitisha. Sisi tumeuliza uongozi wa eneo la kati kuita mkutano wa wanahabari kukanusha maneno ambayo Kuria alisema. Yeye kama ni shahidi wakiwa na Martha Karua waende ICC,” alisema Gikaria.

Gikaria alisesema licha ya kuwa sio wajibu wake kubaini njia inayofaa kufuatwa, kulingana naye, matamshi sawia na ya Kuria yanafaa kutupiliwa mbali.

Tayari Karua ametishia kumfungulia mashtaka Kuria kwa kumhusisha na madai hayo.

Kuria naye amemwambia Karua kwamba yuko tayari kukabiliana naye mahakamani.